1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya SADC vyafanya msako dhidi ya M23

6 Mei 2024

Jeshi la kikanda la jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC likishirikiana na Majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika msako wa waasi wa M23 na washirika wao.

https://p.dw.com/p/4fYbz
Jeshi la kikanda la SADC linalaani kwa nguvu mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa na M23 kwenye Kambi ya waliokimbia vita Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Jeshi la kikanda la SADC linalaani kwa nguvu mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa na M23 kwenye Kambi ya waliokimbia vita Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Vikosi hivyo vimetangaza kufanya operesheni za kuwadhibiti waasi hao ili kulinda amani na usalama na kulinda raia na mali zao dhidi ya vitisho.

Tangazo hili linakuja baada ya mashambulizi ya bomu yaliyotokea tarehe 03 Mei katika kambi za watu waliofurushwa makwao kwenye eneo la magharibi mwa mji wa Goma, ambayo yalisababisha vifo vya watu 16 na kujeruhi watu 35.

Mashambulizi ya mabomu ya Mei 03, wiki iliyopita yameendelea kuzua hisia. Jeshi la kikanda la SADC linalaani kwa nguvu mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa na M23 kwenye Kambi ya waliokimbia vita Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo yalisababisha vifo vya watu 16 na kujeruhi zaidi ya raia 30.

Soma pia: Polisi wa DRC waliochukua nafasi ya Monusco wakabiliwa na hali ngumu

Kupitia ukurasa wao wa X, SADC inabainisha kuwa mashambulizi hayo yaliwalenga raia wasio na hatia, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Wamesema katika taarifa hiyo, "Kulenga kwa makusudi raia wasio na hatia ni ukiukaji dhahiri wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kanuni za haki za binadamu."

Ufafanuzi: Nani yupo nyuma ya mzozo wa Kongo?

Mashambulizi ya waasi wa M23 yalisababisha watu wengi kukimbia, kuziba njia za usambazaji kwenda Goma na kuzorotesha hali ya kibinadamu.

Lakini, Wengi wao wanataka tu kuona amani ikirudi na maisha ya kawaida yakirudi. Justine Bushashire, mkimbizi kutoka Sake, alimpoteza mmoja wa watoto wake kwenye mashambulizi ya mabomu. Amejawa na huzuni na anaamini hakuna faida kuhama kwenda kwenye kambi nyingine ya wakimbizi, bali ni bora amani irudishwe ili waweze kurudi nyumbani.

Soma pia: Viongozi wa nchi za SADC kujadili masuala ya usalama mjini Lusaka

"Jambo muhimu sasa ni kwamba mamlaka zirudishe amani. Mtoto huyu ambaye amefariki alikuwa maalum sana kwangu. Tulikimbia vita, na sasa tulipaswa kuwa salama hapa ; lakini tunauawa. Tumekimbia mvua na tukajikuta baharini. Kuendelea kuishi hapa hakuna faida kwetu. Hatupati msaada wa kibinadamu, badala yake tunakufa. Waache turejee nyumbani," amesema Justine.

Katika eneo lenyewe la shambulizi la mabomu, hofu na taharuki inaonekana kwenye nyuso za wakazi. Baadhi yao wanahamisha hema zao kuelekea maeneo mengine, wakitafuta mahali salama zaidi.
Katika eneo lenyewe la shambulizi la mabomu, hofu na taharuki inaonekana kwenye nyuso za wakazi. Baadhi yao wanahamisha hema zao kuelekea maeneo mengine, wakitafuta mahali salama zaidi.Picha: AUBIN MUKONI/AFP

Mashirika ya kusaidia wakimbizi UNHCR na lile la kushughulikia watoto UNICEF pia wamekemea vikali mashambulizi ambayo yamelenga raia, haswa wanawake na watoto. Kulingana na Angele Dikongue-Atangana, Mwakilishi wa UNHCR huko DRC, "Raia wa mkoa wa Kivu Kaskazini wameshuhudia uvunjifu mbaya zaidi wa haki za kibinadamu kwa zaidi ya miaka miwili katika hii mzozo wa kikatili.

UNHRC imewaomba wote kumaliza ukatili huu usio na maana na kuheshimu takatifu ya maeneo ya kibinadamu yaliyolindwa.

Tangu mapigano yakaribie mji wa Goma, mabomu zaidi ya 10 yamerushwa upande wa magharibi, haswa katika eneo la Mugunga, na kusababisha vifo, majeruhi, na uharibifu mkubwa wa mali ya raia.